Shuhuda

Makumi elfu ya wanawake hukusanyika pamoja ulimwenguni kote kujifunza Neno la Mungu kupitia masomo ya Biblia yaliyotafsriwa na huduma hii ya Mpende Mungu Sana (Love God Greatly).  Baadhi ya wanawake hufanya masomo yetu peke yao ilihali wengine hujiunga na kivundi vya wanawake katika jamii zao na wengine mtandaoni. Kutoka mikoa na vijiji vya Kenya na Tanzania, wanawake huja pamoja sio tu kujifunza Biblia, lakini kuunda jamii zenye upendo na kutia moyo ambazo zinaweza kulea na kukua katika maisha yao ya kiroho.

Ungana nasi katika kusherehekea yote ambayo Mungu anafanya kupitia huduma hii ya Mpende Mungu Sana unaposoma shuhuda kutoka kwa baadhi ya wanawake wetu.

“Wanawake wanapowezeshwa na maarifa ya kweli ya Mungu, dunia inabadilishwa mwanamke mmoja kwa wakati.”

Ester Rwela

Dar es Salaam – Tanzania

Nilizaliwa na kukulia katika familia ya Kikristo, katika kijiji kidogo kinachoitwa Kinyinya, Wilayani Karagwe, Mkoani Kagera, nchini Tanzania. Tulifundishwa kwenda kanisani na kutoa sadaka, ila sikujua kwa nini nilikuwa naenda kanisani na kwa nini nilikuwa natoa sadaka.

Nikiwa high school, nilikutana na rafiki aliyenihubiria Injili ya Yesu Kristo na maisha yangu yakabadilika. Nilitoa maisha yangu kwa Kristo, na tangia hapo nimekuwa nikitembea katika njia za Mungu na kumtumikia. Mnamo mwaka 2006, nilirudi chuoni na, nikiwa huko, nilimtumikia Mungu kama Katibu wa jumuiya ya wanafunzi waliookoka iliyoitwa TAFES (Tanzania Fellowship for Evangelical Students). Kutumika katika jumuiya hiyo ilinisaidia sana kukua kiroho. Tuliwahudumia wanafunzi wenzetu na pia jamii iliyozunguka chuo kupitia uinjilisti. Nilihudumu pia kama mkarimani wa neno la Mungu kwenye ibada za katikati ya wiki na za Jumapili.

Nikiwa nafanya kazi na shirika moja la Kimataifa, nilikutana na mwanamke mmoja aliyeniambia habari za huduma hii ya Mpende Mungu Sana (Love God Greatly) na utumishi wao wa kutafsiri masomo ya Biblia katika lugha mbalimbali. Nilijitolea kutafsiri masomo haya kwa lugha ya Kiswahili. Nilitumika peke yangu bila mtu mwingine kwenye timu yangu kwa miaka kama mitatu. Niliendelea kumwambia Mungu aendelee kunipa nafasi ya kumtumikia na kunipa wengine wa kunisaidia kutafsiri masomo hayo.

Mungu ameleta wanawake na mabinti watano kwenye timu yangu kusaidia kufanya kazi kwenye masomo ya lugha ya Kiswahili. Sote tunaishi katika nchi tofauti tofauti, lakini ni timu. Kupitia huduma hii na kumtumikia Mungu, nimebarikiwa kuwa na marafiki wengi na wazuri na nimemuona Mungu akinipa mahitaji  yangu na kunitunza.Tawi letu linaendelea kukua na kwa sasa tuna wanawake kumi na sita wanasoma Biblia pamoja kwa lugha ya Kiswahili.

Mungu ameendelea kutenda katika maisha yangu, na nimeona akinitendea miujiza. Amenipatia kazi baada ya kukosa ajira kwa kipindi cha miaka mitatu. Amenibariki na jamii nzuri duniani kote na nafasi ya kumtumikia. Sifa, heshima na utukufu ni vya kwake peke yake.

“Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula” (Zaburi 37:25).

Manoti Magati

Geelong – Australia

Kama mtoto nilikimbizwa Hospitali baada ya kumeza sarafu ya senti kumi na ilikwama kooni. Nilipangiwa kufanyiwa upasuaji siku iliyofuata maana mpaka nafikishwa hospitali sarafu ilikuwa imekwama katikati ya mbavu zangu.Usiku huo niliamka na kuhisi kitu mdomoni. Niliingia ndani na kimuujiza ile sarafu ikatoka! Nilijua Mungu alikuwa pamoja nami, na amekuwa na mimi katika mengi zaidi!

Nilimpa Yesu Maisha yangu katika umri wa ujana, na tangu hapo hitaji la moyo wangu imekuwa ni kumuishia yeye. Ninawashukuru wazazi wangu walionilea katika njia za Mungu. Nilioana na mwanaume mzuri, mwenye hofu ya Mungu nikiwa na umri kati ya ishirini na tumebarikiwa kuwa na watoto watatu wazuri.

Tulihamia Australia mnamo mwaka 2014. Baada ya kuja Australia, sikuweza kupata kikundi kizuri cha kujifunza Biblia. Ilikuwa changamoto kupata kundi ambalo lingeendana na ratiba yangu yenye familia iliyokuwa inakua, hivi nilianza kutafuta kundi la kusoma Biblia mtandaoni.Niliipata hii huduma ya Mpende Mungu Sana mnamo mwaka  2017 wakati nipojiunga kwenye somo la Timotheo 1 & 2.

Ninapenda kutumia masomo ya Biblia ya huduma hii ya Mpende Mungu Sana maana ninaweza kusoma Biblia kwa kina nikiwa peke yangu na kujiunga na wanawake kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu. Mtindo wa tafakuri/ SOAP unanichangamotisha kutumia kile nilichokuwa nakisoma na unanisaidia kupata hekima na ufahamu zaidi. Maisha yangu yana utajiri kwa ajili ya jamii hii nzuri. Nimependelewa kuwa sehemu ya timu ya watu wanaotia moyo wengine kwenye huduma hii ya Mpende Mungu Sana na pia kwenye timu ya wakarimani.Mungu amenisaidia kufanya kazi na dada zangu wazuri wa Afrika ya Mashariki kukarimani masomo ya Biblia katika lugha ya Kiswahili. Kama mtoto na mtu mzima, huwa siku zote najihisi kuwa Mungu alikuwa na mimi. Ninabarikiwa kushirikisha matumaini hay ana kutiwa moyo na wanawake ulimwenguni. Nashukuru kwa zawadi ya uzima na wokovu.

Jiunge na Jumuiya Yetu

Huduma ya Mpende Mungu Sana huanza na mpango rahisi kwa kusoma Biblia, lakini hatuishii hapo. Tunapenda kukusanyika katika nyumba na makanisa ndani ya nchi, wakati wengine wanaungana mtandaoni na wanawake duniani kote.