Makumi elfu ya wanawake hukusanyika pamoja ulimwenguni kote kujifunza Neno la Mungu kupitia masomo ya Biblia yaliyotafsriwa na huduma hii ya Mpende Mungu Sana (Love God Greatly). Baadhi ya wanawake hufanya masomo yetu peke yao ilihali wengine hujiunga na kivundi vya wanawake katika jamii zao na wengine mtandaoni. Kutoka mikoa na vijiji vya Kenya na Tanzania, wanawake huja pamoja sio tu kujifunza Biblia, lakini kuunda jamii zenye upendo na kutia moyo ambazo zinaweza kulea na kukua katika maisha yao ya kiroho.
Ungana nasi katika kusherehekea yote ambayo Mungu anafanya kupitia huduma hii ya Mpende Mungu Sana unaposoma shuhuda kutoka kwa baadhi ya wanawake wetu.
“Wanawake wanapowezeshwa na maarifa ya kweli ya Mungu, dunia inabadilishwa mwanamke mmoja kwa wakati.”
Nilijiunga na Love God Greatly kupitia dada yangu ambaye alikuwa msimamizi wa ukurasa wa Facebook wa Love God Greatly Kenya. Yeye alitambulishwa katika huduma hii na rafiki wa familia, na kwa kuwa alijua nilikuwa na hamu ya kujihusisha na jamii inayomcha Mungu, alinialika. Mafunzo ya Biblia na mazungumzo tuliyokuwa nayo kwenye kikundi yalikuwa ya kutia moyo sana, na kweli ilikuwa jamii niliyohitaji. Pia, kwa kuwa ilikuwa ya mtandaoni, ilifanya iwe rahisi sana kushiriki wakati wowote na kutoka mahali popote.
Kukulia katika familia ya Kikristo, nilijihusisha na shughuli za kanisa tangu nilipokuwa mdogo. Katika umri wangu wa ujana, nilikuwa sehemu ya huduma ya vijana, nikifundisha na pia kwenye timu ya sifa na kuabudu. Hata hivyo, nilijitenga na kanisa baada ya kifo cha mama yangu wakati tulipopata uchungu mwingi kutoka kwa chama cha wanawake (women’s guild) ambacho mama yangu alikitumikia kwa miaka mingi.
Binti yangu alipofikisha umri wa miaka miwili, niligundua kuwa sikuwa nikimtendea haki kwa kutompeleka kanisani kujifunza njia za Bwana kama wazazi wangu walivyofanya kwangu. Mithali 22:6a Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha hata atakapokuwa mzee. Kwa hivyo, nilitafuta kanisa lililokuwa na Shule ya Jumapili nzuri, na tulihudhuria uaminifu, lakini nilikuwa tu mtu wa kwenda kanisani bila mabadiliko ya ndani. Miaka miwili baadaye, katika mkutano wa wanawake kanisani, Bwana aliniguza moyo baada ya mwanamke mmoja kuzungumza kuhusu maumivu yaliyofichwa nilianza kuangalia maisha yangu kwa njia tofauti na nikawa makini zaidi kuhusu kuomba na kusifu.
Nilirejesha maisha yangu kwa Kristo mnamo Mei 2015 katika tamasha la kuabudu la Don Moen la Worship at the Gates lililofanyika Mombasa.
Njia ya SOAP ya kujifunza neno la Mungu imekuwa rasilimali muhimu zaidi kutoka Love God Greatly kwangu. Nimeweza kuwaonyesha wanawake wengine ninaoshirikiana nao jinsi ilivyo rahisi kujifunza neno la Mungu kwa kutumia njia hii. Nimeweza kushiriki hadithi za kwenye blogu pamoja na maandiko na wanawake wengine ili kuwatia moyo mara kwa mara kadiri niwezavyo.
Kupitia funzo la Biblia, nimeweza kujifunza mengi zaidi kuhusu neno la Mungu na pia kushiriki hayo hayo na wanawake kutoka kanisani kwangu, hasa wakati funzo linapogusa huduma husika. Kwa miaka mingi, nimeona wanawake wakitiwa moyo na hadithi za wanawake mbalimbali na kupata tumaini kwamba hakika Mungu pia anafanya kazi katika maisha yao.
Kama mwanachama wa timu ya tafsiri ya LGG ya Kiswahili, nimeguswa na kubadilishwa sana kwa kuwa sehemu ya jamii yangu ”jamii inayoomba na mimi na kwa ajili yangu. Tunaweza kujifunza neno pamoja, kujifunza kutoka kwa mwingine, na kutiana moyo wakati mmoja wetu anapojisikia kuvunjika moyo.
Janet Omulindi.
Nilizaliwa na kukulia katika familia ya Kikristo, katika kijiji kidogo kinachoitwa Kinyinya, Wilayani Karagwe, Mkoani Kagera, nchini Tanzania. Tulifundishwa kwenda kanisani na kutoa sadaka, ila sikujua kwa nini nilikuwa naenda kanisani na kwa nini nilikuwa natoa sadaka.
Nikiwa high school, nilikutana na rafiki aliyenihubiria Injili ya Yesu Kristo na maisha yangu yakabadilika. Nilitoa maisha yangu kwa Kristo, na tangia hapo nimekuwa nikitembea katika njia za Mungu na kumtumikia. Mnamo mwaka 2006, nilirudi chuoni na, nikiwa huko, nilimtumikia Mungu kama Katibu wa jumuiya ya wanafunzi waliookoka iliyoitwa TAFES (Tanzania Fellowship for Evangelical Students). Kutumika katika jumuiya hiyo ilinisaidia sana kukua kiroho. Tuliwahudumia wanafunzi wenzetu na pia jamii iliyozunguka chuo kupitia uinjilisti. Nilihudumu pia kama mkarimani wa neno la Mungu kwenye ibada za katikati ya wiki na za Jumapili.
Nikiwa nafanya kazi na shirika moja la Kimataifa, nilikutana na mwanamke mmoja aliyeniambia habari za huduma hii ya Mpende Mungu Sana (Love God Greatly) na utumishi wao wa kutafsiri masomo ya Biblia katika lugha mbalimbali. Nilijitolea kutafsiri masomo haya kwa lugha ya Kiswahili. Nilitumika peke yangu bila mtu mwingine kwenye timu yangu kwa miaka kama mitatu. Niliendelea kumwambia Mungu aendelee kunipa nafasi ya kumtumikia na kunipa wengine wa kunisaidia kutafsiri masomo hayo.
Mungu ameleta wanawake na mabinti watano kwenye timu yangu kusaidia kufanya kazi kwenye masomo ya lugha ya Kiswahili. Sote tunaishi katika nchi tofauti tofauti, lakini ni timu. Kupitia huduma hii na kumtumikia Mungu, nimebarikiwa kuwa na marafiki wengi na wazuri na nimemuona Mungu akinipa mahitaji yangu na kunitunza.Tawi letu linaendelea kukua na kwa sasa tuna wanawake kumi na sita wanasoma Biblia pamoja kwa lugha ya Kiswahili.
Mungu ameendelea kutenda katika maisha yangu, na nimeona akinitendea miujiza. Amenipatia kazi baada ya kukosa ajira kwa kipindi cha miaka mitatu. Amenibariki na jamii nzuri duniani kote na nafasi ya kumtumikia. Sifa, heshima na utukufu ni vya kwake peke yake.
“Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula” (Zaburi 37:25).
Huduma ya Mpende Mungu Sana huanza na mpango rahisi kwa kusoma Biblia, lakini hatuishii hapo. Tunapenda kukusanyika katika nyumba na makanisa ndani ya nchi, wakati wengine wanaungana mtandaoni na wanawake duniani kote.